Habari
WADAU WATAKIWA KUUNGANISHA NGUVU KUPAMBANA NA UKATILI
Wadau mbalimbali wa kupambana na ukatili wa kijinsia wametakiwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili kupambana na kutokomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia nchini.
Wito huo umetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima akizindua kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika viwanja vya Leaders, mkoani Dar es Salaam Novemba 26, 2022.
Waziri Dkt. Gwajima amesema Wadau wakiendeea kufanya kazi kila mmoja bila kuungana vita ya ukatili itakuwa ngumu kuikabili kwa sababu inaweza kuwaacha wengi nyuma.
"Kamati za MTAKUWWA, Polisi jamii, Vijana, Viongozi wa Dini, Mabaraza ya Watoto, Mtandao wa Wanawake, Wazee, Wanaume, Skauti, SMAUJATA na wengine wakiungana mwaka huu adui ukatili ataondoka. Tusipotambuana tutafanya kazi bure,tujue nani yupo wapi na anafanya nini" amesema Mhe. Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Dkt Gwajima amesema Kaulimbiu ya mwaka huu isemayo 'Kila Uhai Unathamani! Tokomeza Mauaji Na Ukatili Dhidi Ya Wanawake Na Watoto' inaikumbusha jamii wajibu wa kuchukua hatua kutokomeza vitendo vyote vya ukatili wa kijinsia ili kuokoa Maisha ya wanawake na Watoto
Ameongeza kuwa, Wadau wanapoungana, ni vema wabuni na kukubali mbinu mpya za kuwasilisha elimu na uhamasishaji kwa kuvunja ukimya kwani ni katika ukimya ndiyo sehemu ya jamii hasa watoto fahamu zao zitakuwa hazielewi kuwa hicho wanachotaka kufanyiwa ni kitu kibaya au kinawapelekea kwenye ukatili mbaya.
"Kwenye kupambana na ukatili wa kijinsia, pamoja na kuungana, ubunifu haukwepeki na uhusika wa jamii yenyewe nao haukwepeki, ni muhimu kwenye kufikia suluhusho la kudumu" amesema WaziriDkt. Gwajima.
Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima amezindua msafara wa Kampeni ya twende pamoja ukatili sasa basi utakaopita katika mikoa 12 Tanzania Bara kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi husu vitendo vya ukatili na madhara yake.
Akitoa salam za Wadau, Mkurugenzi wa Shirika la WILDAF, Anna Kulaya amesema, Wadau wameamua kushirikiana na Serikali kuangazia ukatili ndani ya jamii ambao matokeo yake ni madhara makubwa.
"Mfano ripoti ya uhalifu ya polisi ya mwaka 2021 inaonesha jumla ya watu 29373 wameripoti kufanyiwa ukatili kwa kipindi cha Januari hadi Desemba ambapo zaidi ya kesi 20,000 ni wanawake" amesema Anna Kulaya.
Naye Dkt. Monica Mhija, Mwenyekiti wa Bodi ya WILDAF amewasilisha maombi nane yakiwemo ya kufanya marekebisho ya sheria jambo ambalo, Waziri Gwajima amesema tayari Serikali imeanza kufanyia kazi baadhi ya maombi hayo.
MWISHO