Habari

Imewekwa: Jan, 19 2024

WABUNGE WATAKA HALMASHAURI KUREJESHA MIKOPO YA WDF ILIYOLENGA KUWANUFAISHA WANAWAKE

News Images

WABUNGE WATAKA HALMASHAURI KUREJESHA MIKOPO YA WDF ILIYOLENGA KUWANUFAISHA WANAWAKE

Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Ustawi wa Jamii imeishauri Serikali kuweka mfumo imara wa kuhakikisha Halmashauri zilizopata mikopo ya Mfuko wa Maendeleo wa Wanawake (WDF) zinarejesha fedha hizo ili na wengine wanufaike.

Hayo yamebainika Januari 19, 2024 wakati wa kikao cha Kamati hiyo na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kilichopokea taarifa ya mfuko huo, jijini Dodoma.

Akizungumza katika kikao hicho Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe. Fatma Toufiq ameielekeza Wizara kuweka mifumo thabiti ili kuhakikisha wanufaika wa mikopo hiyo inarejeshwa kwa wakati ikibidi wajiongoze na kufuatiliana wao wenyewe.

"Lazima ufanyike utaratibu ili deni lilipwe. Kwa nini tusiendelee kuhamasisha uundwaji wa vikundi vya ushirika ambao wanawake wenyewe wanakuwa na uongozi wao na kupata mafunzo, halafu mikopo ielekezwe kwenye vikundi hivyo?". Amehoji Mhe. Fatma.

Kwa upande wake Mjumbe wa Kamati hiyo Mhe. Katani Katani amesema mikopo ya wanawake inatakiwa kuthaminiwa kwani wanawake wamekuwa ni waaminifu katika kurejesha. Amesema atahakikisha wanawake katika jimbo lake waliokopeshwa na mfuko huo wanarejesha fedha hizo, kwani zimewasaidia kuinuka kibiashara hasa uuzaji wa korosho nje ya nchi.

Akijibu hoja za Wajumbe wa Kamati hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha kwamba, jitihada za kurejesha mikopo hiyo zinaendelea na kwa mwaka huu 2024 Wizara itahakikisha Maafisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Halmashauri wanasimamia urejeshaji wa mikopo hiyo.

"Suala la mikopo hii tunakwenda kulisimamia tujue ilipokwenda, kuna madawati sita kwenye Halmshauri zetu ikiwemo Dawati linaloratibu uwezeshaji wanawake kiuchumi na jamii, watatwambia. Tunapokea ushauri wa kwenda kuviimarisha vikundi kupitia Maafisa Maendeleo ya Jamii." Amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Awali akiwasilisha taarifa ya mfuko wa WDF Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru amesema mfuko huo uliokuwa unaratibiwa na Wizara kupitia Halmashauri kabla ya mabadiliko ya mwongozo mwaka 2022, changamoto ni baadhi ya wanufaika kutorejesha mikopo hiyo baada ya kukopeshwa ambapo hadi sasa deni lililopo ni shilingi milioni 574.118 zilizotolewa na Wizara kwa Halmashauri ili Halmashauri hizo ziwakopeshe wanawake. Aidha shillingi milioni 497.112 zilizotolewa na wizara mwaka 2022 kwa vikundi pamoja na wanawake mmoja mmoja zinaendelea kurejeshwa.

MWISHO