Habari

Imewekwa: Nov, 26 2022

​RUAHA KUANZA KUFANYA TAFITI ZA LISHE MANISPAA YA IRINGA

News Images

Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilichopo mkoani Iringa kimepata Kibali cha kufanya tafiti za hali duni ya lishe kwenye Manispaa ya Iringa ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo la udumavu linaloikabili Manispaa hiyo.

Hayo yamebainishwa na Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii,Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, Mwanaidi Ali Khamis alipokipongeza chuo hicho kwa kuaminiwa na kukabidhiwa jukumu husika, wakati wa Mahafali ya 14 ya Chuo hicho Novemba 26, 2022.

Mhe. Mwanaidi amesema ni wakati muafaka wa tatizo hilo kutafutiwa ufumbuzi wa kudumu.

"Napenda kuupongeza uongozi wa Chuo hiki kwa kushirikiana na wadau wengine kufanikiwa kupata kibali cha kufanya utafiti wa hali ya Lishe katika Manispaa ya Iringa, ninauagiza uongozi wa chuo kuhakikisha mnafanya tafiti nyingi juu ya changamoto za kijamii" Amesema Mwanaidi

"Naviagiza vyuo viandike machapisho mbalimbali ikiwemo Majarida ya Kitaaluma na maandiko mengine yenye tija ambayo yanavifanya vyuo hivi viwe na hadhi kama vilivyo vyuo vingine vilivyofanikiwa kupitia tafiti na Maandiko mbalimbali yenye lengo la kukitangaza chuo pamoja na kuijulisha jamii ni nini chuo kinafanya" Ameongeza Mwanaidi.

Kuhusu suala la Ukatili, Mhe. Mwanaidi amewaasa Wahitimu hao 606 kwenda kushirikiana na Wanajamii katika kusukuma mbele gurudumu la Maendeleo huku akiwataka wakawe Mabalozi kwenye Kupinga Ukatili.

Akisoma taarifa ya Chuo Mkuu wa Chuo hicho Boniphace Mafungu ameishukuru Serikali kwa fedha ya Ukarabati na Ujenzi, ikiwepo ujenzi wa ukumbi wa mihadhara utakaogharimu shilingi za kitanzania milioni 100 mpaka kukamilika kwake na itakuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 260 kwa awamu moja.

Mafungu amesema fedha nyingine walizopokea ni kwa ajili ya ujenzi wa Maktaba ya kisasa itakayo gharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni 200 na kuwa na uwezo wa kuchukua wanachuo 144 kwa awamu moja .

"Hatuna Maneno mazuri ya kushukuru lakini itoshe kusema vilevile tunaendelea na ujenzi wa mabweni mawili unaogharimu kiasi cha shilingi za kitanzania milioni mia 300 ikiwa shilingi milioni mia 150 kwa kila moja na uwezo wa kuchukua wanachuo 128 kwa awamu moja kwa majengo yote mawili" Alisema Mkuu huyo wa Chuo.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Chuo amemwambia Naibu Waziri kuwa, Chuo kimefanya ukarabati wa jengo la Ubunifu lenye ofisi za ugavi, chumba cha Ubunifu, ukumbi mdogo wa mikutano na jiko la uokaji) kwa gharama ya shilingi za kitanzania milioni 83

Mkuu huyo wa Chuo hakusita kueleza baadhi ya changamoto zinazo wakabili ikiwepo Njia kwa ajili ya Wanafunzi wenye Mahitaji Maalum pamoja na Uchakavu wa Nyumba za Watumishi, changamoto ambazo Naibu Waziri aliahidi kuzichukua na kuzifanyia kazi.

Kwa upande wake mmoja ya Mhitimu Bahati Sigi kutoka mkoani Mwanza aliyehitimu Ngazi ya Stashahada ameahidi kutumia Elimu aliyopata katika kutatua changamoto za Jamii.

"Hapa tumejifunza dhana ya uanagenzi na mimi nilibobea hasa kwenye Ufugaji wa Samaki kwangu mimi hii nitaitumia kama fursa kwa kushirikiana na Jamii" Amesema Sigi.

Chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha kilianzishwa mnamo miaka ya 1960 kwa kutoa mafunzo ya kilimo kikiwa chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu na Mwaka 2002 Chuo kilibadilishwa kutoka Chuo cha Kilimo na kuwa Chuo cha Maendeleo ya Jamii na kuanza kutoa mafunzo ya ufundi katika fani mbalimbali zikiwemo za Useremala, Uashi, Ushonaji, Ufundi Magari, Upishi, Ufundi Umeme wa Majumbani na Mbinu bora za Kilimo.

MWISHO